Imewekwa: 29 Dec, 2025
Bodi ya Kahawa Yazindua Ugawaji wa Zaidi ya Miche Milioni 6 ya Kahawa Wilayani Mbinga

Meneja mkuu wa chama kikuu cha ushirika wilaya ya Mbinga MBiFACU, Ndugu Faraja Michael Komba, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa zaidi ya miche milioni 6 ya kahawa ya ruzuku kwa wakulima na wazalishaji wa zao hilo wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 23 Desemba, 2025, ambapo Ndg. Komba ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya kahawa (TCB) amesema Bodi ya Kahawa imejipanga kikamilifu katika utoaji wa miche hiyo bila malipo kwa lengo la kuwapunguzia wakulima gharama za ununuzi wa miche na kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Ndg. Komba alieleza kuwa awamu hii bodi imeweka mikakati madhubuti ya ufuatiliaji ili kuhakikisha miche yote inayogawiwa inapandwa katika maeneo husika, tofauti na changamoto zilizojitokeza awali ambapo baadhi ya wakulima walishindwa kupanda miche au kuiuza kwa wakulima wengine.

“Awamu hii bodi imejipanga kufanya ufuatiliaji wa kutosha ili kuhakikisha miche yote inayogawiwa inapandwa katika maeneo yaliyokusudiwa,” alisema Ndg. Komba.

Kwa upande wao, wakulima wa kahawa wilayani Mbinga wameishukuru Serikali kwa kuandaa zoezi hilo, wakisema litachochea ongezeko la uzalishaji na kuboresha kipato chao.

Miongoni mwa wanufaika, Bw. Laxford Haule, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia miche bora ya kahawa, akisema hatua hiyo ni chachu ya maendeleo kwa wakulima.

“Hatua hii itatusaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chetu. Tunaomba juhudi hizi ziendelee ili wakulima wa Mbinga na Tanzania kwa ujumla wanufaike zaidi na zao la kahawa,” alisema Haule.

Wanawake nao wameendelea kushiriki kikamilifu katika kilimo cha kahawa. Bi. Maria Mbunda, mmoja wa wakulima walionufaika na zoezi hilo, amesema kupata miche bure kumempa hamasa kubwa ya kuendeleza kilimo cha kahawa.

“Ninawashauri wanawake wenzangu kutumia fursa hii ya kupata miche bure ya kahawa ili kujiongezea kipato cha familia na kuchangia kukuza uchumi wa Taifa,” alisema Bi. Mbunda.

Kwa mujibu wa takwimu za sekta ya kahawa, mauzo ya kahawa ya Tanzania katika soko la kimataifa yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 140 hadi zaidi ya Dola milioni 230, sambamba na kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 34,000 hadi kufikia tani 85,000 mwaka jana.